KWELI NNE ZA MSINGI

3/10/2003

(Maneno haya yalinenwa papohapo na waumini watatu kwenye halaiki ya ushuhuda ya kipentekoste, katika kituo cha kijiji fulani Afrika. Kwa siku moja tu usharika mzima ulivutika kwa Yesu kimsingi na kamwe haujatazama nyuma tangu hapo. Kwa gharama kubwa ya kibinafsi, mabadiliko mengi yalifanyika yakaleta mgeuzo wa kudumu kwa watu wengi na hata kwa muundo wao wa kiuchumi, katika kijiji hicho. Kwa muda wa saa chache tu habari zilisambaa katika eneo lao hilo miongoni mwa vikundi vingine vya dini, kwamba kulikuwa na tukio maalumu la kimungu. Laiti kama ingekuwa inawezekana kuyahifadhi yaliyosemwa na ndugu wenyeji wa kijiji hicho cha Afrika katika saa zilizofuatia kulishwa neno la Bwana kwa waongoka hao. Kwa kweli ilishangaza na kutia moyo kuona ujasiri na ari yao kwa Nyumba ya Baba vilivyodhihirishwa na kupenda ukweli na matendo mema katika siku zilizofuatia siku hiyo.)

Kuna hazina ambayo ni mwamko wa watu wa Mungu ulimwenguni kote sasa hivi. Ni azma yetu kuwaachia nyinyi hazina hiyo na kuwapa tumaini ambalo mtaenenda nalo maisha yenu yote. Hata kama mngelikuwa wachache hapa kijijini kwenu, na nyinyi kwa kweli si wachache … kama Jonathan, rafiki mpenzi wa Daudi, alivyowahi kusema, Mungu hazuiwi kuokoa na wingi au uchache wa watu. Kadhalika Mungu alisema, yeyote apewaye tumaini hana budi kuonyesha uaminifu. Tungependa kuwaonyesheni mambo machache ambayo yatabadilisha maisha yenu na kubadilisha jinsi kanisa linavyodhihirishwa ili kumwinua juu zaidi Mfalme wetu, Yesu na kutimiza matarajio yake. Hizi ni hazina maalumu ambazo siku zote zimekuwamo ndani ya bibilia. Ni tumaini letu kwamba kwa nuru ya Roho Mtakatifu, macho yetu yote yatafunguka kuziona kweli hizi maridadi. Ukweli huu wahusu jinsi Mungu anavyotaka kujenga Nyumba yake ili sote tuweze kuwa imara zaidi pamoja. Anataka kuijenga Nyumba yake ili malango ya jehanama yasiweze kuishinda tena. Anataka kuijenga nyumba yake yote hivi kwamba mahusiano yetu yapate tiba. Anataka kuijenga nyumba yake ili awe huru kutibu miili yetu, nyoyo zetu na roho zetu. Anataka kuijenga nyumba yake ili tuwe imara na tuwe na hekima ili Habari Njema za Yesu ziweze kuenea zikiwa na nguvu zaidi kuliko zilivyopata kuwa wakati wowote mwingine.

Je Mnao ujasiri wa kuyasikia mambo haya? Mtalitii neno la Mungu mnapoyasikia mambo haya? Mtayageuza maisha yenu bila kujali gharama? Kama mnao ujasiri wa kutii na kuwa tayari kwa lolote, basi tafadhalini kaeni tuzungumze. Tuizungumzie hazina hii ya kweli nne za msingi.

Kunazo kweli nne ambazo ni lazima tujenge juu yake. Bila hizi Nyumba ya Mungu haitakuwa imara kamwe na malango ya jehanama yataendelea kuifanya Nyumba ya Mungu mahali pa vurumai. Bali tukiyaelewa na kuyatii mambo haya manne, na tukiwa tayari kwa lolote kwa ajili ya kweli hizi za Mungu, basi Mungu naye ataiheshimu hali hiyo na kuupeleka uwezo wake katika maisha yetu. Maskini watatajirika na wanyonge watakuwa na nguvu. Huo umekuwa siku zote upendo na matakwa ya Mungu. Lakini, hazina hii imeporwa kutoka kwetu tokea karne ya kwanza na kuendelea. Tumepokonywa mengi sana na desturi tupu za binadamu.

Ukweli wa Kwanza: Nini maana ya Mkristo?

Ukweli wa kwanza wa kimsingi ni kufasili vizuri “maana halisi ya Mkristo ni ipi?” Tumekuwa hobelahobela sana juu ya jambo hili ulimwenguni kote na katika kila utamaduni. Kwa vile hatujaielezea wazi hata maana ya “Mkristo ni nini, tumeijenga sehemu kubwa ya Nyumba ya Mungu mchangani. Tumekifasili kinachomfanya mtu mkristo kwa vitu kama mawazo, jazba au malezi ya kifamilia. Tumeifasili maana ya Mkristo ni nini kutokana na hali ya kuwa mtu ana seti “sahihi” za imani. Tumemfasili mtu kuwa mkristo kutokana na kuimba kwake vizuri, au kuwa na mahudhurio ya kutosha na kutoa zaka kikamilifu. Hivyo sivyo Yesu alivyofasili ukristo.

Yesu alisema “kama hutelekezi yote huwezi kuwa mfuasi wangu”. Yesu alisema “kama huubebi msalaba wako kila siku huwezi kunifuata.” Katika kitabu cha Matendo ya Mitume, Biblia yasema Wafuasi waliitwa “Wakristo” kwanza kule Antioch. Kwa hivyo kila uonapo neno mfuasi katika mafundisho ya Yesu akilini mwako fikiria neno “Mkristo”. Yesu aliposema kama hutelekezi yote huwezi kuwa mfuasi wangu, alikuwa anamaanisha kwamba huwezi kuwa Mkristo kama hujikusuru maisha yako. Hakusema “kama huudhurii ibada/mafundisho huwezi kuwa Mkristo”. Yesu alisema “kama hujikusuru uhai wako mwenyewe huwezi kuwa Mkristo”. Yesu anawaita watu watakaojifia nafsi zao wenyewe. Wao watatelekeza kila kitu na kumfuasa. Wataipa kisogo dhambi yao ya binafsi na wataupa kisogo ubinafsi wao. Watawapenda wengine zaidi ya vile wanavyojipenda. Mahusiano haya na Yesu yatageuza jinsi watendavyo kila siku ya Mungu.

Tusipofasili neno “Mkristo” kama Yesu afanyavyo Nyumba ya Mungu itadidimia mchangani na kutokomelea mbali. Jambo hili ndilo Yesu Mfalme aliloahidi kwamba litatokea kama tukijenga katika mchanga wa kusikia na kuimba na kusema na ilhali hatutii. Nyumba tutakayoijenga pengine itatufurahisha sisi, lakini itakuwa ni kazi bure kwa Yesu. Nyumba tunayojenga inaweza ikatufurahisha kidogo kwa sababu tunaimba na kukutana na wenzetu, lakini haina maana yoyote kama Mungu hapendezwi nayo. Haina maana yoyote kama shetani bado ni mshindi katika mapambano maishani mwetu. Kama hatujengi maisha na kanisa liletalo furaha kwa Yesu, basi tunapoteza wakati wetu na wa Mungu.

Matokeo Makubwa

Jiwe la kwanza la msingi katika kujenga Nyumba ya Mungu ni kutoa wasifu wa Mkristo kama Biblia inavyoutoa. Ni lazima tuamue kulingana na kile Mungu anachokiita Mkristo. Je mtu aweza kuwa msharika wa kanisa la Mungu na asiwe Mkristo? Hata kidogo! Lakini ulimwenguni kote watu wanafundishwa kwamba ni sawa kwa wakristo na wasio wakristo kuwa washarika wa kanisa. Biblia yasema hii si halisi. Katika1 Wakorinto 5, Biblia yasema, “Ondoa chachu kutoka kwenye donge.”

Ondoa dhambi kutoka kwenye kanisa. Ni muhimu sana kulielewa hili, kwa sababu Mungu alisema, chachu ndogo yalichachusha donge zima.

Je mwakumbuka wakati kuta za Jeriko zilipoboromoka chini? Watu wa Mungu walikuwa na nguvu kwa njia ya kimungu. Basi mara tu baada ya kuta za Jeriko kuanguka, Israeli ilishindwa vitani. Walikanyagwakanyagwa! Kwa nini Israeli haikufua dafu vitani? Kulikuwa na mtu mmoja Israeli nzima aliyekuwa na dhambi rohoni mwake. Mungu alichukia kwa sababu mtu mmoja katika kanisa zima alikuwa na dhambi katika maisha yake iliyokuwa imefichika. Huyo mtu, Achan, alikuwa na sanamu iliyofichwa ndani ya hema lake. Mungu aliiacha Israeli yote ishindwe vibaya sana vitani kwa sababu mtu mmoja alikuwa na dhambi katika maisha yake. Mungu ni yule yule jana, leo na milele, Amina? Hadi leo Mungu huchukia sana watu wa nyumbani mwake na kanisani mwake wanapokuwa wanaficha dhambi katika maisha yao. Jambo hili huvunja moyo wake. Biblia yasema Mungu hushusha hukumu juu ya hili.

Je ni sawa kwetu kusema kwamba mtu ambaye hajawahi kujitolea maisha yake kikamilifu kwa Yesu anaweza kuja na kuwa mmoja wapo wa washarika wa kanisa? La hasha! Hili ni kosa kubwa sana! Mungu huishusha hukumu yake juu ya nyumba nzima kwa sababu ya huyo mmoja anayejidai kuwa Mkristo na hali kamwe hajawahi kuyatoa maisha yake kwa dhati kwa yesu. Kwa hivyo kama twataka kuiona Nyumba Tukufu Itendayo kazi ya Mungu, jambo la kwanza tunaloposwa kulifanya ni kuifasili maana ya jina Mkristo kama vile Yesu anavyolifasili. Maandiko Matakatifu yasema, “Bila kuyatelekeza yote huwezi kuwa mfuasi wangu.” “Kama unampenda baba na mama na watoto zaidi yangu huwezi kuwa mfuasi wangu.” Ukiipenda duania na anasa za dunia umekuwa adui yangu. Mungu huwapinga wenye kiburi na kuwabariki wanyenyekevu.

Tunapaswa kufasili kwa usahihi maana ya ukristo. Hatuna budi kumfasili kwa usahihi msharika wa kanisa hasa ni nani. Huwezi kujigamba kuwa eti umekogeshwa na kuwa sehemu ya mwili wa Yesu pamoja na watu hawa na kujitia eti wewe ni Mkristo kama moyo wako si mali ya Yesu uwapo nyumbani, au kazini, au shambani. Kama mahusiano yako si mahusiano matakatifu huna budi kutubu na kuyatolea maisha yako kwa Yesu.

Ukweli wa Pili: Uongozi ni Nini?

Jambo la pili ambalo tunapaswa kulifasili, jiwe la pili la msingi katika kujenga Nyumba ya Mungu, linahusu maana ya uongozi katika Nyumba ya Mungu. Huu ni ukweli wa ajabu! Jambo hili litakusisimua na kugeuza maisha yako. Katika nchi zote duniani kote sote tunafanya kosa kubwa sana kuhusu uongozi katika kanisa. Tumeona kwamba mara nyingi kule India na katika nchi nyingine ni mtu mwenye baiskeli na anayejua kusoma ambaye huchaguliwa kuwa kiongozi. Huku Marekani yule anayekwenda kujifunza Biblia katika Seminari au shule za Biblia, au ambaye ni mfanya biashara hodari, au mzungumzaji mzuri, ndiye huwa kiongozi au “mchungaji”. Hii si njia ya Mungu! Uongozi wa Mungu hautegemei nani anajua kusema, nani mjuzi sana, au nani ni msemaji hodari sana, au nani ana ujuzi mkubwa sana katika biashara.

Kama Yesu

Nitawapeni mfano kutoka katika Maandiko Matakatifu. Katika matendo 6, kulikuwa na wajane ambao walikuwa na njaa sana mara nyingine kwa sababu walisahauliwa. Chakula kilipogawanywa, kulikuwa na wanawake wa Ugiriki ambao walisahauliwa na hawakutunzwa vizuri. Kanisa la Yerusalemu lililazimika kulitafutia ufumbuzi tatizo hili. Ukisoma Biblia yako utagundua kwamba kulikuwa na njia fulani ya kuwachagua watu hao. Iliwabidi kuwachagua baadhi ya watu wa kulitatua tatizo hili. Je, Biblia inasema, wachagueni watu saba miongoni mwenu wanaozijua Biblia zao? La hasha! “Wachagueni watu saba miongoni mwenu wanaoweza kuimba vizuri?” La hasha! “Wachagueni watu saba miongoni mwenu wenye ujuzi wa biashara au waliomo katika biashara ya chakula?” La hasha! Wachagueni watu saba miongoni mwenu ambao ni wazungumzaji hodari sana?” La hasha! Njia ya kulitatua tatizo hilo ilikuwa “kuwachagua watu saba miongoni mwenu waliojawa na Roho Mtakatifu na wenye kujawa na hekima”.

Hawa walikuwa watu waliopambana na majaribu ya kila siku. Hawa hawakuwa watu waliokwenda chuoni kuwa wacha Mungu, au watu walioweza kuzungumza vizuri tu. Hawa walikuwa watu waliokuwa marafiki wa Mungu na marafiki wakubwa wa kila siku kwa ndugu zao. Stefano na Filipo na wale watu saba walikuwamo majumbani mwa watu kila siku wakijaribu kuwasaidia. Walikuwa wakiwatekea maji waumini wengine. Walikuwa wakiwapa mikono watoto wa rafiki zao, wakizungumza nao na kuwafundisha. Walikuwa wakiwatembelea watu nyumbani kwao walipokuwa wamekata tamaa. Walikuwa wakiwatembelea watu mchana kazini kwao ili kuwapa moyo. Na wala hawakuwa eti viongozi! Walikuwa ndugu wa kawaida tu walioyaishi maisha ya Yesu kila siku. “Wachagueni miongoni mwenu watu saba wanaofanana na Yesu; watu saba wanaoweza kumwona Mungu na kumsikia Mungu. Wachagueni watu saba wanaoiosha miguu ya waongofu kila siku. Watu saba wa kawaida kabisa wanaompenda Mungu sana moyoni mwao na wenye kuonyesha mshikamano wa Kimungu na maisha, kwa kuwa watu hawa hufanana na Yesu kila siku majumbani mwa watu, basi twajua wamejawa na Roho Mtakatifu. Hawakujawa na Roho Mtakatifu kwa sababu wanaweza kupiga makelele zaidi, au kuimba vizuri zaidi, au kusema mambo mengi zaidi. Wamejawa na Roho Mtakatifu wa Yesu kwa sababu wanafanana na Yesu katika maisha yao ya kila siku. Huu ndio uongozi pekee katika Biblia. Katika Agano Jipya Yesu aliwaambia wale Mitume kumi na wawili wasimwite mtu yeyote mwalimu ; msimwite mtu yeyote baba. Msimwite mtu yeyote kiongozi; msimwite mtu yeyote bwana; msimwite mtu yeyote rabi, msimwite mtu yeyote mchungaji; msimwite mtu yeyote mheshimiwa, kwani nyinyi nyote ni ndugu. Kwa hivyo, basi, sasa tunayo sura tofauti ya uongozi.

Tofauti na Ulimwengu

Kujifunza jambo hili kulikuwa kugumu sana kwangu mimi binafsi. Miaka mingi sana iliyopita nilikuwa “mchungaji” mpaka nilipotambua kuwa Biblia ilisema kwamba nilitarajiwa kuwa tu ndugu miongoni mwa ndugu nikitumia kipaji ambacho huenda nilijaliwa kuwa nacho “miongoni mwao kama mtu atumikiaye” na siyo kama Bwana mkubwa au mtu wa kusujudiwa wakati wote.

Kama hiyo ni kweli kwa Petro na Yohani na kama ni kweli kwa Yakobo na Mitume wengine, ni lazima iwe kweli kwangu mimi pia! “Nyinyi nyote ni ndugu tu.” Mimi niliyatelekeza mapesa tele niliyokuwa nimeyachuma katika biashara kuwa “mchungaji”—-—na sasa ilinibidi kuyaacha mapesa na cheo cha “mchungaji!” Niliwajibika kuamua kuwa nitakuwa ndugu miongoni mwa ndugu. Chochote ambacho Yesu alikuwa amenitendea katika maisha yangu kingelijidhihirisha majumbani na katika maisha ya wengine ninapokuwa nikishika mikono ya watoto. Haikuwa lazima niendelee kuwa mtu mkubwa. Haikuwa lazima niendelee kuwa kiranja. Niliweza tu kutenda yale Paulo aliyosema aliyatenda na Watesalonike, na Wafilipi na Waumini wa mji wa Korintho.—-—Yaani kuwapenda watu kama baba, na rafiki, na kama ndugu toka nyumba hadi nyumba.

Paulo alisema, nilienda toka nyumba hadi nyumba nikiwa na machozi. Yeye aliwapenda watu kama baba na kama ndugu. Aliyalea maisha yao kama mama amleavyo mtoto. Waumini wengine nao walimfanyia hivyo hivyo. Huu ndio uongozi katika kanisa la kweli la Agano Jipya.

Yesu aliwaambia Mitume, “ Watu wa Mataifa wana njia fulani za kupata uongozi, bali hivyo sivyo ilivyo kwenu nyinyi.” Katika kanisa la kweli, kanisa ambalo Malango ya Jehanamu hayawezi kulishinda, uongozi ni tofauti sana na ule wa njia za kidunia. Uongozi unatoka ndani na siyo wa kujitwisha kwa mabavu tu kwa nje.

Vipaji na Mamlaka

Acha niwachoree picha. Biblia yasema katika Waefeso 4 kwamba Yesu alipopaa mbinguni aliwapa watu vipaji. Yesu alichukua vipaji vyote alivyokuwa navyo (na Yesu alikuwa na vipaji vingi vya kiroho, sivyo?) na akavikabidhi kwa watu wake kwa pamoja. Hakuvichukua vipaji vyote alivyokuwa navyo na kuvibwaga kwa mchungaji. Hakuvichukua vipaji vyote na kumpa “eti mtu mmoja wa Mungu. Maandiko matakatifu yanasema alivichukua vipaji vyake vyote na kuvikabidhi kwa mwili wake wote. Biblia yasema Roho imemiminwa na kutolewa kama zawadi kwa kanisa zima, kama vile Roho apendavyo. Kama wewe kweli ni Mkristo; kama umeyaacha maisha yako ya anasa kwa ajili ya Yesu, basi Roho Mtakatifu anakupa zawadi maalumu kabisa. Kipaji chako ni sehemu ya Yesu.

Kabla Yesu hajarudi mbinguni alisema, “Mamlaka yote mbinguni na duniani ni yangu.” Je, mwakumbuka Yesu alisema hivyo? Mamlaka yote ni yake Yesu siyo ya mtu mwingine yeyote! Kwa hiyo, kama Yesu alijitoa sehemu yake kwako, sehemu kwa huyu, na sehemu kwa yule, basi katika vipaji vyovyote vya kimungu alivyomjalia kila mmoja wenu kunayo mamlaka katika vipaji hivyo. Yesu ndiye alivitoa vipaji hivyo, naye anayo mamlaka yote.

Biblia yaorodhesha vipaji vya aina nyingi. Kwa mfano, Roho Mtakatifu alitupa neema ya huruma kama kipaji. Kipaji cha huruma ni sehemu ya Yesu aliyowapa watu fulani. Ni kipaji cha kimungu. Sisi sote inatubidi tuwe na huruma ya kimungu ambayo ni kipaji cha Roho Mtakatifu. Mamlaka yote ni yake Yesu. Kwa hivyo, kama alikupa kipaji maalumu cha huruma, basi wewe umepewa kipaji cha Kimungu cha huruma na mimi sinacho, ikiwa mamlaka yote ni yake Yesu nawe unayo sehemu hiyo ya Yesu basi mimi ninakitukuza kipaji hicho ndani mwako. Unayo mamlaka kwa upande huo. Unaelewa? Hii ndiyo maana halisi ya uongozi. Mamlaka yote ni yake Yesu. Sisi sote tunavyo vipaji vyetu maalumu, na Biblia yasema ni lazima tupeane nafasi. Biblia yasema kunavyo vipaji vya kufundisha. Waebramia 5 inasema, ingalitupasa sisi sote tuwe tumeshakuwa walimu mpaka sasa. Waefeso 4 na Warumi 12 zasema kuna vipaji vya Kimungu vya kufundisha anavyovitoa Yesu. Kwa hivyo kunayo mamlaka katika kipaji hicho, kwa sababu ndiye anayekitoa, na yeye ana mamlaka yote. Hata hivyo kufundisha ni kipaji kimojawapo tu na sehemu moja tu ya Yesu. Kunavyo vipaji vingine vingi. Kila kipaji alicho nacho kila mmoja wenu ni sehemu ya Yesu. Mamlaka yote ni ya Yesu, basi na tuviheshimu vipaji vilivyomo ndani mwa kila mmoja wetu. Hakuna eti mamlaka fulani maalumu yaliyomo ndani mwa mtu mmoja “wa Mungu” na wengine wote wabakie kukaa na kutazama tu. Ila kutokana na vile ambavyo wanaadamu wamelijenga na kuliendesha kanisa kwa muda wa miaka 1700, tumeendesha mambo kana kwamba kuna kipaji kimoja tu—kipaji cha uchungaji. Lakini hicho ni kipaji kimojawapo tu! (Au kana kwamba huenda kila mtu mwingine yeyote amekirimiwa kipaji cha kutoa pesa tu!”) Kuna mamia ya vipaji kwa sababu Yesu alijitoa kikamilifu kwa Familia yake. Hii ndiyo sababu Yesu alisema sisi sote hatuna budi kuwa ndugu miongoni mwa ndugu. Tunavihitaji vipaji vya kila mmoja wetu. Tunavihitaji vipaji vyote vya Yesu. Tukijenga vibaya sote tunakula hasara. Ikiwa mtu mmoja tu atasukumwa mbele kuwa ndiye mchungaji na wengine wote wakae na kuwa wasikilizaji tu wakati wote, basi hakuna yeyote atakayenufaika na kipaji chako wewe au chake yeye. Watu watanufaika na vipaji vya mchungaji tu. Na hiyo ni kidogo mno. Kama tunataka kuona ukubwa wa Mungu, kama tunataka kuona maisha yetu yote yanabadilika, na maisha ya watoto wetu yanabadilika, tunamhitaji Yesu katika ukamilifu wake. Tusiridhike na sehemu tu ya Yesu. Amina?

Ujarisi wa kubadilisha na ujasiri wa kuongoza

Je mnaelewa sasa kwa nini nilisema hapo awali ya kwamba hamna budi kuwa na ujasiri? Mambo ni lazima yabadilike! Hamwezi kuendelea kuyafanya yale ambayo siku zote mmekuwa mkiyafanya. Itawabidi mwamue kuvitumia zaidi vipaji vyenu. Itawabidi mwamue kuwa watii na kuwa wajasiri. Kama mtaamua kukaa kitako kimya vitini mwenu tu muda wote bila ya kuvitumia vipaji vyenu zaidi ya vile ambavyo mmekuwa mkifanya, vipaji vyenu vitaendelea kuzorota. Yeyote yule aliyejaliwa amana au karama fulani hana budi kuwa mwaminifu. Je, mnakumbuka yaliyompata yule mtu aliyeizika talanta yake? Yesu alisema, mtumishi mbaya na mzembe we! Hiyo ndiyo pia kauli yake kwetu tusipotenda yale tunayopaswa kutenda. Nisipokitumia kipaji changu, au wewe usipokitumia kipaji chako, sisi tu wabaya na wazembe.

Je, mnaona jinsi desturi za watu zinavyoiba na kulipora neno la Mungu? Je, ingelikuwaje kama ungelikuwa mkimbiaji wa Olympiki na tukakufunga ukiwa umelala kitandani? Tungalikuwacha hapo, hata kama ungelikuwa mwanariadha staid, misuli yako ingalisinyaa na ungalikufa. Uwezo wako wote ungalipotea kwa sababu umefungiwa kitandani maisha yako yote. Hali kadhalika jinsi ambavyo tumekuwa tukiendesha shughuli zetu katika Nyumba ya Mungu kwa muda wa iaka 1700, imewafungia vitandani watu wa Mungu walio wengi. Hawajaweza kuamka kukimbia na kutimiza wito wao kwa sababu tumeendesha mambo vibaya. Tukijenga au kuendesha kwa njia ambayo inamwinua juu mtu mmoja au “watumishi wa kanisa” tu, na kuvikausha vipaji vya wengine, sisi ni wahalifu mbele ya mahakama ya mbinguni. Kwa kawaida, haikuwa kwa sababu watu ni wabaya ndiyo tukaendesha mambo vibaya. Bali mara nyingi imetokana na kwamba hatukujua jinsi ya kuijenga vyema Nyumba ya Mungu.

Jiwe la kwanza la msingi wa kweli ni kwamba wakristo halisi tu wanaweza kujiita washarika wa kanisa. Jiwe la msingi ni kwamba ni lazima tuielewe vizuri maana ya uongozi. Tumemweka madarakani mtu mmoja tu kwa miaka 1700. Tumekichukua kipaji kimoja tu, kipaji cha “mchungaji” (au mlishi kwa tafsiri nzuri zaidi” na kukifanya kipaji kikuu. Hiyo imekuwa mbali kabisa na hali halisi kanisani na katika Biblia! Na sasa vilevile haiwezi kuwa halisi. Hali hii imewafungia kwa kamba watu wa Mungu kitandani hivi kwamba hawajaweza kuwa (watu) wale Mungu aliowaita kuwa. Uongozi umo ndani ya watu wote wa Mungu. Biblia yatuita ufalme wa makasisi. Biblia haisemi ufalme wenye makasisi, bali ufalme wa makasisi. Hakuna kundi moja tu maalumu kama la makasisi wa Kilawi wa Agano la kale. Katika Agano Jipya watu wa Mungu wote wanatarajiwa kuwa makasisi kila mmoja kwa wengine. Mungu alisema “Ufunuo utakapomjia wa pili, BASI WA KWANZA NA AKETI!” Kama umejaa Roho Mtakatifu na umejaa hekima, basi wewe ni kiongozi. Hoja si kwamba umesoma au kwamba unasema vizuri sana; si kwamba wewe ni mwanaume au mwanamke, au kijana au mzee. Kiongozi ni mtu mwenye kipaji cha Yesu na aliye na uhusiano na Yesu uliojaa Roho Mtakatifu na uliojaa hekima. Uongozi ni kuishika mikono ya watoto kila siku. Uongozi ni kuvitibu vidonda vya watu wa Mungu toka nyumba moja hadi nyingine kila siku. Uongozi ni kusaidia kuyatatua matatizo katika maisha ya watu kila siku. Uongozi ni kuiosha miguu ya watu kila siku. Hiyo ndiyo maana ya uongozi. Hiyo ndiyo aina pekee ya uongozi ambayo Biblia inaiongelea—yaani kuitumia ile sehemu ya Yesu ambayo Roho aliitia ndani mwa kila mmoja wetu, na hiyo ndiyo pia sehemu ya uongozi na mamlaka yetu. Hii maana yake ni kwamba hatuna budi kubadili jinsi tunavyofanya mambo sasa hivi. Tunapaswa kubadili jinsi tunavyoutazama uongozi. Tunapaswa kubadili jinsi tunavyoendesha uongozi.

Huu ni mtazamo wa kimapinduzi sana. Mtazamo huu utabadilisha utaratibu wetu mkutanoni. Utabadilisha utaratibu katika maisha yetu ya kila siku. Na kuna gharama yake. Kuna gharama ambayo hatuna budi kuilipa. Lakini Mungu anatutunza mara mia kwa lolote tunalojitolea, kwa mujibu wa ahadi ya kweli ya Yesu.

Nilipokuwa “mchungaji” niliamua kubadilisha maisha yangu. Niliamua kwamba nitasadiki na kutii yasemayo Maandiko juu ya Uongozi. Nilichagua kuwa ndugu miongoni mwa ndugu na siyo mbele ya ndugu. Nilikuwa na wasiwasi. Nilikuwa na wasiwasi nitatunzaje familia yangu. Niliogopa kwamba pengine ningejitenga na Mungu. Nilikuwa na wasiwasi kwamba huenda watu wasiniheshimu tena. Nilikuwa na wasiwasi juu ya mambo mengi. Lakini nilijua lile alilolisema Mugnu katika Biblia. Yeye alinitaka niwe ndugu miongoni mwa ndugu. Katika maisha yangu ya kila siku nisingekuwa bwana mkubwa tena. Ningebakia tu kuwa mmoja wapo wa wanandugu na bado nikaweza kuvitumia vipaji vyangu kutoka kwa Yesu kama “ndugu miongoni mwa ndugu zangu”, ambao vilevile wanavitumia vipaji vyao. Hali hii ilibadilisha kila kitu kwangu, lakini Mungu alikuwa mwaminifu kabisa kabisa. Aliahidi kwamba hakuna mtu yeyote yule ambaye alipata kujitolea kitu chochote asiweze kurudishiwa mara mia moja au zaidi ya kile alichojitolea. Mungu hutunza ahadi zake! Amina?

Duara kukizunguka kiti cha Enzi

Katika harakati za utendaji, moja ya mambo tunayoweza kubadilisha mara moja ni jinsi tunavyokaa tuwapo pamoja. Hili linaonekana jambo la kijinga sana, lakini ni jambo muhimu sana. Nitawapa mfano kutoka katika maandiko. Katika Marko 32 na 34, Maria na watoto wake walikwenda kumtafuta Yesu. Walipofika mlangoni pa mahali Yesu alipokuwa na watu wa Mungu. Akaambiwa, “Yesu, mama yako na kaka zako na dada zako wapo pale nje”. Je, mnakumbuka jibu la Yesu lilikuwa nini kwa taarifa hiyo? Aliwaambia wale waliokuwa wamekaa katika duara kumzunguka, “mama zangu na kaka zangu na dada zangu ni nani?” Tazama, walikuwa wamekaa kumzunguka! Si kufanya hivyo ndiko kulikuwa jambo la kawaida kabisa tunapokuwa tumekusanyika kumsikiliza yeye, na siyo tu mtu mwenye vipaji vya kawaida tu? Bila shaka!

Nataka kupendekeza kwamba kama kweli tunataka kuheshimu vipaji vilivyomo ndani mwa kila mmoja wetu, kama kweli tunataka kuvidhihirisha vipaji vyote vilivyomo ndani mwa watu wa Mungu wote, kuna mambo mengi tunayopaswa kubadili. Jambo mojawapo linaweza kuwa jinsi tunavyokaa katika mikutano yetu ya pamoja. Yesu alipokuwapo hapa duniani, alikuwa na duara la watu waliomzunguka. Jambo hili linaweza likaonekana jepesi sana kwenu, linaweza hata lisionekane jambo muhimu sana kwenu, lakini mimi nawahakikishieni ni muhimu.

Mtu kazini au sokoni akikwambia kitu, je jinsi anavyokisema ni muhimu? Bila shaka ni muhimu! Kama wakikwambia huku wameketi au kuegemea nyuma ya jiwe, na kusema kwa kunong’ona wakipiga miayo, ni tofauti sana na kukwambia kitu hicho hicho wakiwa wamekukabili uso kwa uso na huku wamekukazia jicho kali. Jinsi jambo lolote linavyosemwa ni muhimu sana. Tukikaa tumeangalia mbele sote tunamkazia macho mtu mmoja tu. Hapo, sisi si watu sawa miongoni mwa watu sawa tena. Mimi niko chini ya mtu yeyote yule aliyekalia kiti cha enzi mbele yangu kama bwana mkubwa wangu au rubani, au mwendeshaji au askari wa barabarani (trafiki), au mtaalamu wa “darasa” au “huduma” fulani. Lakini sikilizeni hili kwa makini! Mtumishi halisi wa Mungu hajitafutii sifa zake binafsi. Mtu mkuu kuliko wote aliyepata kuzaliwa na binadamu mpaka wakati huo, Yohani Mbatizaji alisema, “Yesu anapaswa kuongezeka, kwa utukufu, nami napaswa kupungua.” Kila mtu mwaminifu kwa Mungu anasema vivyohivyo, “Yesu, anapaswa kuongezeka kwa utukufu, nami napaswa kupungua. Sipendi kujivutia makini kwangu peke yangu. Sipendi wakati wote watu wanitazamie mimi peke yangu tu kuwa ndiye mtu mwenye majibu yote. Sifurahii kuwa ndimi pekee msemaji wakati wote. Mimi hamu yangu ni kumpenda na kumtumikia Yesu, na kuwasaidia watu wengine wote kufanya hivyo. “Yesu yabidi aongezeke kwa utukufu, nami yabidi nipungue.”

Kila mtu mwaminifu kwa Mungu anahitaji kumpisha Yesu apate sifa zaidi kuliko yeye. Jambo hili pia baadhi ya watu wataona halina maana, bali mimi nawahakikishieni, baada ya kuzitembelea nchi nyingi na miji mingi, hili si jambo dogo. Jinsi tunavyosema kitu ni muhimu kabisa. Tukipanga viti kwa safu badala ya mviringo, tumekaa kumzunguka Yesu, ni kama kumbwagia sifa zote mtu mmoja, watu wengine wote wakabakia kuwa wasikilizaji tu na kivutio kikawa mtu huyo mmoja tu. Hilo ni kosa kubwa, kwani kunavyo vipaji vingi miongoni mwetu, na nyote ni sehemu sawa na Yesu. Tukielekeza viti vyote mbele, tunakitukuza kipaji kimoja tu. Mnaonaje kama tukivipangua viti hivi na kuvipanga katika duara hivi kwamba kila mtu awe akimwelekea mwingine na Yesu awe katikati? Kwa njia hiyo vipaji vyote vitapewa nafasi sawa. Kumbukeni kwamba Biblia yasema, “kwa wale waliokaa katika duara kumzunguka Yeye…hawa ndio mama zangu, kaka zangu, dada zangu,”. Huenda kuna mtu mwenye kipaji cha mchungaji amekaa kwenye kiti hiki katika duara hili, pengine kuna mtu mwenye kipaji cha mwalimu amekaa hapa na mwenye kipaji cha rehema amekaa pale. Mtu mwenye kipaji cha msaada huweza kuwa amekaa hapa; wakati mwenye kipaji cha unabii amekaa pale. Vipaji vyote ni sawa, kwa kuwa vipaji vyote ni Yesu. Je, hili linaeleweka?

Basi, katika duara hili, kama mama analia juu ya kuwalea wanawe, mtu mwenye kipaji cha ualimu anaweza kusema na ndugu huyu na kumfundisha yale ayasemayo Paulo katika Timoteo juu ya wanawake. Mtu mwenye kipaji cha huruma anaweza akamtia moyo dada huyu kwa kumpa fikira za huruma; pengine yeye pia alipata kuwa na watoto wadogo wakati mmoja na angeweza kumwelezea hisia zake juu ya jambo hilo. Na mtu mwenye umaizi wa kinabii angeweza kupenya ndani ya moyo wa dada huyu na kuona kwa nini ana matatizo na watoto wake, na kadhalika. Basi, sasa HATIMAYE, tunaweza kulitii agizo kutoka kwa Mungu, ya kwamba, “Ufunuo ukimjia mtu wa pili, basi WA KWANZA NA AKETI!” Aleluya!! (kelele zikapigwa!)

Kila Mmoja Muhimu Sawa

Katika Wakorintho 14 Mungu alisema pia, mjumuikapo pamoja, kanisa zima likiwa pamoja, ndugu zangu, basi kila kitu na kitendeke kwa kujenga mwili. Kila mmoja wenu analo neno la fundisho, wimbo, ufunuo. Hakuna bwana mkubwa mmoja isipokuwa Yesu! Msimwite mtu yeyote kiongozi, bwana, mwalimu au mchungaji. Nyinyi nyote ni ndugu. Nyinyi nyote mnaye Yesu. Yesu ni sawa ndani mwa kila mmoja wetu. Wakati fulani tunahitaji rehema ya Yesu. Mara nyingine tunahitaji mafundisho ya Yesu. Na mara nyingine tunahitaji wimbo wa Yesu. Na mara nyingine tunahitaji msaada wa Yesu kutatua matatizo. Lakini mara zote ni Yesu peke yake.

Je, mnaweza kuona sasa kwamba jambo hili linahitaji ujasiri? Mnaweza kuona jambo hili linahitaji imani na utii? Je, mnaweza kuona kwamba jambo hili litayageuza maisha yenu mkianza kuishi kwa maadili haya? Hamtakuwa mmefungiwa kitandani kwa kamba tena! Kipaji chako hakitarudishwa nyuma tena. Kipaji chako ni sawa tu na changu, ila tu ni tofauti. Mimi ninakihitaji kipaji chako kama vile wewe unavyokihitaji kipaji changu.

Baadhi ya mambo muhimu kabisa ambayo yamepata kutokea maishani mwangu yametokea kwa sababu mtoto mwenye umri wa miaka kumi na miwili aliyekuwa na kipaji fulani aliyageuza maisha yangu. Wanawake huathiri maisha yangu. Watu huathiri maisha yangu. Wazee huathiri maisha yangu. Na hii siyo Jumapili asubuhi tu, bali ni kila siku. Ufalme wa makasisi . Kila siku. Mikutano ni kitu cha ziada tu, kwa kweli asilimia tisini ya kukua kwetu inatokana na kuishi kwetu pamoja, hiyo ina maana kwamba ni lazima mtoke nje ya nyumba zenu na mwingie kaya za wengine. Mnawaletea maji nyumbani kwao, mnawaletea chakula, mnawaletea mavazi yumbani kwao. Mkiona wamemkasirikia mtoto, inaweza kuwalazimuni kuwavuta kando mzungumze nao; zungumzeni nao na tembeeni nao. Mkiona kiburi katika maisha yao washikeni mikono na kuwasihi wasiwe na kiburi. Ukiona choyo katika maisha ya ndugu fulani, mzungushie mkono na useme “tafadhali usiendelee kuwa na choyo.” Hatufumbi macho tu mpaka mkutano ujao. Tunaishi ndani ya maisha ya kila mmoja wetu kila siku kama makasisi tukiifanya kazi ya Mungu. Hili pia ni agizo halisi kutoka kwa Mungu, katika Waebrania 3 na sehemu tele nyingine. Itikeni wito wa kuwa wenzi; tianeni shime na kupeana ushauri mwema kila siku ya Mungu; ili sote tusalimike na kupotoshwa na kufanywa wagumu na dhambi, wakati mchana ungalipo. Ni lazima tuliongelee jambo hili mara nyingi zaidi.

Jiwe la kwanza la msingi ni “maana ya Mkristo ni nini. Nini maana ya Msharika wa kanisa?” Kama mnao watu katika kanisa ambao hawajamwongokea Yesu kikweli kweli, basi daima mtakuwa na vita na ugonvi wa mara kwa mara ambao si lazima muwe nao. Biblia yasema, tangu mdogo kabisa, hadi mkubwa kabisa wote watamjua yeye. Kila mmoja anayejiita msharika ampendaye Yesu kwa dhati, huwa na amani sana—hapana ugonvi, hapa umbeya. Na kuna kupendana kwingi kila siku. Huwezi kuwa msharika halisi wa kanisa la Yesu mpaka umeyakana hata maisha yako kabisa. Ni Wakristo tu wanaoweza kuwa washarika wa kanisa. Mtu mwingine yeyote ni mpita njia tu, lakini si msharika wa kanisa la Yesu. Hii ndiyo kauli mahsusi ya Biblia. Na chachu haina budi kuondelewa kwenye donge vinginevyo hatumpendi Yesu kama tunavyosema. “Kama unanipenda utayatii maagizo yangu.” Kanisa ni la kuunganisha, kuimarisha, kuandaa na kuwakinga wale waliooshwa katika damu yake, wakishachagua kuzifia nafsi zao ili wamkumbatie Bwana Yesu, daima. Yeyote yule ambaye hajakata shauri kama inavyodhihirishwa na maisha yake na machaguo yake na kama “anaupenda mwanga” (Yohani 3, Yohani 1) kama yalivyo mapenzi ya Mungu, basi huyo asijihesabu katu kuwa Mkristo au sehemu ya mwili wa Kristo. Fasili nyingine yoyote ya kanisa imebuniwa na watu, na “malango ya Jehanama bila shaka yataliangusha kanisa hili bandia. Tazameni kwa makini, mtaiona hali hiyo katika pembe ya kila mtaa toka mji hadi mji, taifa hadi taifa. Huo sio mpago wa Mungu, bali kitu tu cha kuridhisha mwili wa binadamu, wakati jina la Yesu linatumika kupoza dhamira. Lakini hakuna kupoa hapo! Masiha hupatembelea pale tu anapoweza kusimika nguzo ya taa yake!

Jiwe la pili la msingi lahusu uongozi. Roho na uhai wa sasa wa Yesu Mfufuka—ndicho kiongozi chetu pekee. “Ulimwengu hautaniona, lakini nyinyi mtaniona”. Kipimo cha Roho huyo ambacho mtu yeyote anacho, kipaji ambacho mtu anaweza akawa nacho, kule kukomaa na undani hasa wa kuwiana kiuhai na Yesu mzima ambako mtu anako—hiyo ndiyo fasili ya Biblia ya “Uongozi.”

Ukweli wa 3: Maisha ya kila siku

Jiwe la tatu la msingi linahusu maisha yetu ya pamoja ya kila siku. Tumeshazungumza kidogo juu ya maisha yetu ya pamoja ya kila siku. Maisha ya kila siku hayategemei katu kuna mikutano mingapi, bali jinsi gani tunajihusisha na maisha ya kila mmoja wetu. Je, tunajihusisha kila siku kama makasisi katika ndoa za jirani zetu, na watoto wa jirani zetu, na tabia za kazini na dalili za mienendo ya jirani zetu? Je, tunajihusisha kila siku, kwa dhati, na ndugu zetu? Je, “tunabebeana mizigo na hivyo, kuitekeleza Sheria ya Kristo? Je, tunatubiana dhambi zetu kila mmoja kwa mwenzake na hivyo kuponyeshwa? Je, “tunapambana kama mtu mmoja kwa ajili ya Imani,” tukiwa tumeegemeana na kusukwa pamoja na kila iungo tulichokiegemea, na hatukubali chochote pungufu yake kama “kanisa halisi” na MWILI HASA WA KRISTO? NI KATIKA HILO TU nitabaini kile Yesu alichomaanisha aliposema, nitajenga kanisa langu ambalo malango ya Jehanama hayatawezakulishinda au kulihimili!” Kila kitu kingine ni nyumba iliyojengwa katika mchanga wa kutaka kuridhisha tu, uliyopooza, wenye utovu wa utii, ulio na utengano na utoaji wa vijisababu. Na, kwa bahati mbaya, itazaa matunda yanayoistahili. Mungu alisema jinsi tunavyojenga ni muhimu!

Nitawapeni somo moja la maandiko, lakini litayageuza maisha yenu mkilitii. Mkilizingatia somo hili moja, mtashangaa jinsi mambo mengine haya yote yatakavyoleta maana. Ni nguzo kutoka kwa Yesu. Je mtalitekeleza? Mtalitekeleza? Je, mnampenda? Kutenda asemayo kutayageuza maisha yetu yote, kuliko tu kulikubali analolisema, au kulisoma, au kuliimba, au kulifanyia mkutano. Hebu, na tulitazame pamoja kwa lugha yenu. Andiko lenyewe liko katika Waebrania 3:12-14.

“Jihadharini, basi rafiki wapendwa. Hakikisheni kwamba mioyo yenu si miovu, isiyoamini na yenye kuwageuza kutoka kwa Mungu Mzima. Ni lazima mtahadharishane kila siku, mradi inaitwa ‘Leo’, ili pasiwe na yeyote miongoni mwenu atakayehadaiwa na dhambi na kuwa mgumu dhidi ya Mungu. Kwani tukiwa waaminifu hadi mwisho, na tukimwamini Mungu kwa nguvu kama wakati tulipoanza kuamini tutashiriki katika yote yaliyo ya Kristo.”

Zingatieni yanavyosema maandiko. Neno hili latoka kwa Mungu mwenyewe. Mungu Mwenyezi asema ni lazima tutahadharishane, KILA SIKU. Ni lazima tuambatane kila siku. Roho Mtakatifu alilichagua neno “kila siku”. Hakusema kila Jumapili. Hakusema kila Jumapili na kila Jumatano. Na wala hakusema mikutanoni. Alisema jihusisheni na maisha ya kila mmoja wenu KILA SIKU. Kama hamfanyi hivyo, Mungu alisema, mtakuwa wagumu zaidi wa mioyo msiweze kuhisi jinsi Yeye anavyohisi, na mtadanganyika mkadhani kwamba mnajua yaliyosahihi na hali hamyajui. Hakuna kusema tu myatende. Bali alisisitiza kwamba kutoyatenda mambo hayo kutawaumizeni sana. Kama sina ndugu wanaoniongelesha kila siku juu ya maisha yangu, kila siku nitakuwa mgumu. Nitadanganyika. Unaweza kusema, “lakini mbona nasoma Biblia yangu kila siku!” “Lakini mbona nasali kila siku?” Mke wangu ni Mkristo nami humwona kila siku.” Hivyo sivyo Mungu alivyosema. Unaweza kusoma Biblia yako na kusali kila siku, lakini kama hujihusishi na maisha ya kila mmoja wenu kila siku, utakuwa mgumu wa moyo zaidi na zaidi, na mwenye kudanganyika zaidi na zaidi.

Nani aliandika Biblia? Mungu? Mungu aliagiza tujihusishe na maisha ya kila mmoja wetu kila siku. Kama unaniona nakuwa mchoyo, huna budi kunijia na kusema, “Ndugu—usiwe mchoyo. Jambo hili linamhuzunisha Yesu.” Ukiona ninajivuna, tafadhali nisaidie kwa kunikumbusha kwamba Mungu anawapinga wenye majivuno. Mimi sipendi Mungu anipinge. Ni lazima unisaidie kwa sababu mimi mwenyewe siwezi kuiona hali hiyo kila wakati. Hakuna anayeweza. Tahadharishaneni kila siku ili kusiwe na yeyote miongoni mwenu mgumu wa moyo na aliyedanganyika. Hii ni sehemu muhimu ya maisha yetu ya pamoja (na ambayo kwa bahati mbaya inapuuzwa kila siku ulimwenguni kote). Hivi ndivyo wewe unavyokuwa kasisi ukivitumia vipaji vyako. Basi, sasa mnaweza kuona hii haina uhusiano sana na mikutano, sivyo?

Ukweli wa 4: Mikutano

Kwa muda wa miaka 1700 ulimwengu wa kikristo umekanganya masuala. Mkristo ni nani? Kiongozi ni nani? Maisha ya kila siku yanapaswa kufananaje? Jiwe la nne la msingi linahusu mikutano yetu. Mikutano yetu inapaswa kufananaje? Katika hili pia Wakristo wamejenga ovyo kwa miaka 1700. Baba yetu anataka kuwarudishia vitu hivi katika maisha yenu sasa. Na Mungu atageuza maisha yenu kimiujiza na kumgeuza kila mtu aliyepo karibu nanyi, kama matokeo yake. Hizi ni kweli zenye nguvu na thamani kubwa sana. Hata hivyo ni lazima tuthubutu kuwa na mikutano kama Biblia inavyosema katika 1 Wakorintho 14 “Mkutanapo ndugu, kila mmoja ana neno la mafundisho, wimbo, ufunuo”. Hakuna aliye na mamlaka ila Yesu mwenyewe. Tunajumuika pamoja tukishafikiria namna ya kuhimizana kuelekea kwenye upendo na kazi njema. Tunawazia na kuombea jinsi tunavyoweza kusaidiana pindi tukutanapo, na kila mmoja wetu anachukua jukumu la kuwa mwenye kuleta neno la Mungu na Upendo wa Mungu. Kila mmoja wetu “amefikiria namna ya kuhimizana kuelekea kwenye upendo na kazi njema”. Hilo limo katika Waebrania 10. Tafadhalini kuweni na uhakika litazameni andiko linalofuatia! Hili linatuhusu sote, hata “mikutanoni”! 1 Wakorintho 14 yasema “ufunuo unapomjia mtu wa pili, mtu wa pili anaposikia kitu kutoka kwa Mungu, basi wa kwanza na akae kitako.” Hivyo ndivyo isemavyo Biblia. Kwa nini hatutendi isemavyo Biblia? Hakuna mtu maalumu ambaye anatarajiwa kufanya lolote kwa nguvu zake mwenyewe—ila kwa kumsikiliza na kumwitikia Mungu, kama mtu mwingine yeyote. Kama mtu yeyote analeta fundisho kutoka kwa Yesu, na kila mmoja anakuja na neno la fundisho au wimbo, au ufunuo, kama ndugu huyu au ndugu huyu yungali anawashirikisha wengine katika neno alilopewa na Yesu kwa ufunuo na ndugu wa pili naye anapata ufunuo, ndugu wa kwanza hana budi kuketi; kama vile Biblia inavyosema. Biblia imekuwa ikisema hivyo siku zote. Kwa nini hatufanyi hivyo? Tumerithi mzigo mzito wa desturi kutoka kwa Wakatoliki na wahenga wetu. Kumekuwepo na padri au kasisi mbele na halafu wamekuwepo walei—watu maskini wote, wote wasikilizaji, wameketi na kusikiliza tu. Huu ndio mtindo na mafunzo ambayo Yesu alisema anayachukia—ule wa “Manikolaiti” (kwa tafsiri “wale wanaowashinda watu wake”), badala yake, Yesu alitaka “duara la watu walioketi kumzunguka, alisema kwamba kila mmoja ana neno la fundisho, wimbo, ufunuo, na ya kwamba sisi sote ni sawa, sisi sote ni kaka, sisi sote ni dada, tulio na sehemu tofauti za Yesu zilizomiminwa ndani yetu binafsi, kwa manufaa yetu sote. Jambo hili ni jema na la ajabu kabisa! Yeye anatunasua na “desturi tupu tulizozipokea kutoka kwa wahenga wetu” zenye makasisi na walei na kawaida za dini—na kutufanya huru kuingia katika ulimwengu wa hatari na kumwamini na kumpenda yeye kama mboni yetu pekee! Na hapatakuwapo na vurugu hapo kwani yeye anajiita “Mungu wa Amani” na “Utaratibu”. Huo ndio utaratibu wake hasa, na siyo hila za binadamu eti “kwa niaba yake”.

Misingi ya Mabadiliko

Je, utaratibu huu ni tofauti na ule mliozoea? Je tunao ujarisi wa kujenga kwa njia ya Mungu? Je, jambo hili linatisha? Je, hii yaonekana kama njia ya kufurahisha? Njia hii yafurahisha sana! Tumepata kuwa na watu waliokuwa washarika wa kanisa ambalo sisi ni washarika wake—baadhi yao hata walikuwa Wakristo kwa miaka ishirini na tano, na bado walikuwa (kama) watoto wachanga. Lakini walipojifunza njia hizi na kuanza kutenda kama makasisi, walikua kiasi cha miaka kumi katika mwaka mmoja tu. Haleluya! Wengine walikuwa viongozi wa makanisa yaliyokuwa na mamia na hata maelfu ya wafuasi waligundua kwamba walikuwa bado ni watoto wachanga tu kiroho! Walidhani kuwa ni viongozi lakini waligundua kwamba kulikuwa na watoto wa mama wengi ambao walikuwa wamekomaa zaidi kiroho kuliko wao. Basi walilazimika kukua kutoka utoto huo, na wamekua! Yote haya yatisha sana, lakini pia yanasisimua.

Mkizitekeleza kweli hizi ambazo siku zote zimekuwamo ndani ya Biblia zenu, mtashangaa kuona jinsi mtakavyokuwa karibu zaidi na Yesu miaka miwili toka sasa. Onyaneni kila siku. Jihusisheni na watoto, na ndoa, na mahali pa kazi kila siku. ENENDENI HUKO! Ni lazima mziache sehemu zenu za starehe na hadhi na KUENENDA HUKO, jambo ambalo msingeliweza kufanya kabla ya sasa! (Naam, nakuambia wewe!) Tafadhali, kwa jina la Yesu! Zungumzianeni neno la Mungu katika maisha ya kila mmoja wenu, kwa njia ya vitendo, kila siku. Ndugu zangu, mnapojumuika kila mmoja ana neno la fundisho, wimbo, ufunuo. Ufunuo umjiapo mtu wa pili, wa kwanza na aketi. Mnapoliishi neno hili, mnaweza kugundua kwamba baadhi ya wale mliowadhania kuwa Wakristo hawampendi Yesu kwa kiwango kile ambacho siku zote mlikuwa mkifiria wanampenda. Wakati huo huo baadhi ya wale mliowadhania kuwa wazembe walikuwa na nguvu na wenye busara zaidi ya vile ambavyo mngalivyowahi kudhani. Njia za Mungu huumbua udanganyifu na uongo na kuwafanya wanyonge kuwa imara sana. Mungu atukuzwe!

Basi tunawakabidhi utajiri huu na kuwaomba muishi kwa jina la Yesu. Haya mawe ni ya msingi. Hamna budi kufasili Mkristo halisi hasa ni nani. Ni lazima muuelewe uongozi na kile ambacho hasa unapaswa kuwa. Ishini maisha yenu pamoja kila siku, mkitiana shime, mkijengana na kusaidiana kukua na kumpenda Yesu zaidi mchana wenu wote na jioni zenu zote. Njooni mkakutane kwa duara kumzunguka Mfalme Yesu.

Mkimpenda Yesu na kujenga kwa njia iliyo sahihi, malango ya Jehanama hayatazidi kushinda. Dhambi itapondwa. Udhaifu na maradhi vitaponyeshwa. Mahusiano yatajengwa au kurejeshwa, zaidi ya vile ambavyo mtu angeliweza kuota katika ndoto za ajabu. Mtang’ara kama nyota ulimwenguni, huku mkiuonyesha uzuri wa Mungu. Na Bibi arusi, kanisa, “atajiandaa” na kuwa tayari Bwana arusi atakaporudi!! Amina.

jesuslifetogether.com
Kiswahili Languages icon
 Share icon